20 Desemba 2023 - 15:51
HAMAS yaendelea kupinga usimamishaji vita wa muda, yataka Israel ikomeshe vita kwanza

Vyombo vya habari vya Kizayuni vimetangaza kuwa, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAHMAS imepinga pendekezo la kusimamishwa vita kwa muda huko Ghaza na imeendelea kusisitizia msimamo wake wa kukomeshwa kwanza jinai za Israel, kabla ya kufanyika mazungumzo yoyote yale.

Televisheni ya al Alam leo imevinukuu vyombo hivyo vya Kizayuni vikisema kuwa, serikali ya Israel ilikuwa imependekeza kwa Qatar, kufanyike mazungumzo ya kusimamisha vita kwa muda na kuachiliwa huru mateka wengine 40 wa Kizayuni walioko mikononi mwa wanamapambano wa Palestina. 

Vyombo hivyo vya habari vimesema, Waziri Mkuu wa Qatar amewajibu Wazayuni kuwa, sharti la HAMAS ni kukomeshwa kikamilifu vita kabla ya kufanyika mazungumzo yoyote ya kubadilishana mateka.

Huku hayo yakiripotiwa na sambamba na kuendelea mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni hhuko Ghaza, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya kibinadamu ametoa mwito wa kuundwa mahakama maalumu ya kufuatilia jinai zinazofanywa na Israel kwenye vita hivyo.Martin Griffiths, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Kibinadamu amesema kwenye mahojiano kwamba ukiukaji wa sheria katika vita vya Ghaza unaonekana wazi na kuna haja ya kuanzishwa mahakama maalumu kuhu jambo hilo. Utawala wa Kizayuni umekuwa ukiendesha vita vya kikatili katika Ukanda wa Ghaza tokea tarehe 7 Oktoba, vita ambavyo kwa mujibu wa maafisa wa Palestina na duru za Umoja wa Mataifa, mbali na kusababisha maafa ya kibinadamu ambayo hayajawahi kushuhudiwa, vimeharibu miundombinu mingi na kuua shahidi maelfu ya raia, wengi wao wakiwa ni watoto na wanawake. Utawala huo ghasibu bado unaendeleza hujuma zake hizo katika maeneo yote ya Ukanda wa Ghaza ambapo takwimu za karibuni kabisa zinaonesha kuwa zaidi ya Wapalestina 19,400 wameshauawa shahidi na zaidi ya 52,200 wengine wameshajeruhiwa hadi hivi sasa.

342/